logo blog

MFUMO WA UPOKEAJI WA MAOMBI YA KAZI KWA NJIA YA MTANDAO

http://ajirampyatanzania.blogspot.com/
Sekretarieti ya ajira katika Utumishi wa umma inatarajia kuzindua mfumo mpya wa utumaji na upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao kupitia “Recruitment portal” hivi karibuni baada ya hatua za majaribio ya mfumo huo kuonyesha mafanikio.

Sababu za kuanzisha mfumo huu mpya zinalenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi katika kufikisha huduma kwa wateja, kuongeza ufanisi katika mchakato wa ajira, Kupunguza muda wa mchakato wa Ajira ili kukidhi mahitaji ya wadau, kuwafikia waombaji wa nafasi za kazi wengi zaidi, kudhibiti udanganyifu wa sifa toka kwa waombaji wa fursa za Ajira kwa kurahisisha ukaguzi na uhakiki wa taarifa za waombaji  kazi kwa kuunganishwa na mifumo ya taasisi mbalimbali lakini pia kukidhi maelekezo ya Sera mbalimbali za utumishi wa umma pamoja na dira ya Taifa ya mwaka 2025 kuhusiana na umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kutimiza malengo ya Taifa.

Hadi sasa Sekretarieti ya ajira imefanya majaribio ya kupokea maombi ya kazi kwa kutumia mfumo wa “Recruitment Portal” kwa matangazo ya kazi matano ambayo yaliyowahusu waajiri mbalimbali serikalini na muitikio umeonekana kuwa mzuri.

Matangazo hayo yalihusu Wakala wa serikali mtandao lililotolewa tarehe 22 Aprili, 2014 ambapo kati ya nafasi 12 zilizotangazwa idadi ya maombi yaliyopokelewa yalikuwa 1,158, Tangazo la nafasi za Mkemia mkuu wa Serikali lililotolewa tarehe 4 Desemba, 2014 lenye nafasi 11 jumla ya maombi ya kazi 119 yalipokelewa kwa njia ya mtandao.

Matangazo mengine ni ya  Mamlaka ya Hali ya hewa la tarehe 4 Desemba, 2014 lililokuwa na nafasi  moja na idadi ya maombi ya kazi matatu yaliyopokelewa, tangazo la tarehe 16 Januari, 2015 la Wizara ya Ardhi lililokuwa na nafasi 51 ambalo jumla ya maombi ya kazi 738 yaliwasilishwa na tangazo la mwisho lilitolewa tarehe 10 Machi, 2015 kwa niaba ya taasisi mbalimbali Serikalini jumla ya maombi ya kazi 2,567 yalipokelewa kutumia mfumo huu. Idadi hii inaonyesha kuwa watu wengi wameanza kuhamasika na matumizi ya mfumo huu.

Taratibu za uzinduzi rasmi wa mfumo huu inatarajiwa kufanyika hivi karibuni ambapo sekretarieti ya ajira inatarajia kupunguza muda wa uendeshaji wa  mchakato wa ajira kwa asilimia 34%. Aidha mfumo pia utapunguza changamoto kadhaa zikiwemo baadhi ya barua kutofika kwa wakati au kupotea kwa kutumia njia ya posta, Mrundikano wa barua na nyaraka nyingine zinazohusiana na maombi ya kazi  kutokana na matumizi ya karatasi, Barua za vibali vya ajira kuwasilishwa wakati vimechelewa na kusababisha mchakato kuchelewa na gharama inayotokana na uendeshaji wa mchakato mzima wa ajira kuwa juu.

Pia mfumo huu utakuwa rafiki na rahisi kwa watumiaji kwa kuwa wataweza kutumia simu zao za kiganjani kupata taarifa za mchakato wa ajira kila wakati kwa kupiga *152*00#
Tunatoa rai na kusisitiza kuwa waombaji kazi na wale wanaotarajia kuingia katika soko la ajira wajisajili katika mfumo huu kwa kufungua http://portal.ajira.go.tz ili kuingiza taarifa zao za kitaaluma, wasifu binafsi (CV) pamoja na vyeti.

Matarajio ya Sekretarieti ya ajira ni kuona kuwa mara baada ya mfumo huu kuzinduliwa rasmi utaongeza ufanisi, ubora, uwazi na uwajibikaji wa huduma zinazotolewa, kupunguza muda unaotumika sasa wa kuendesha mchakato wa ajira, Gharama za uendeshaji zitapungua kwa kiasi kikubwa na mfumo utawafikia waombaji wa fursa za kazi wengi zaidi na kwa haraka.

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inapenda kuwasisitiza wananchi hususani waombaji kazi kuwa inaendelea na uimarishaji wa mfumo mpya wa kutuma maombi ya kazi kwa njia ya mtandao (recruitmemnt portal) ili kuondoa baadhi ya changamoto zilizojitokeza baada ya majaribio kabla ya uzinduzi wake na tunasisitiza na kuhimiza waombaji kazi pamoja na wanafunzi wanaotarajia kumaliza vyuo waendelee kujisajili katika mfumo huo mpya.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma.